TFF yaikata maini Yanga

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa endapo Yanga itaendelea na msimamo wake wa kukataa udhamini wa kampuni ya Azam Media ambayo imepewa haki ya kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu ya Bara katika televisheni, klabu hiyo haitapewa mgawo wowote wa fedha na kwamba udhamini huo hautavunjwa.

Hata hivyo, Yanga kupitia kwa katibu mkuu wake, Lawrence Mwalusako, ilisema jana kuwa klabu hiyo iko tayari kukaa mezani na kujadili upya udhamini huo ili wapatie fedha zinazolingana na hadhi ya klabu hiyo inayoshikilia ubingwa wa ligi hiyo.

Akizungumza na NIPASHE, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, alisema kuwa shirikisho halitarudi nyuma kuhusiana na udhamini huo na wanashangazwa na kauli ya Yanga kuukataa wakati wajumbe wake walishiriki katika vikao vyote vilivyofanyika kabla ya kusaini mkataba na Azam Media.

Karia alisema pia Yanga kwa kuukana udhamini huo wanapaswa kufahamu kuwa hali hiyo inachangia kukimbiza kampuni nyingine zilizokuwa na nia ya kudhamini soka nchini.

"Tutaendelea mbele na wao kama watashikilia msimamo wao tutawaacha, kama tutasikiliza maamuzi yao (Yanga) na wanachama wao, je klabu nyingine 13 nazo tutazifanyaje, haitakuwa sahihi kufanya kwa klabu moja," Karia alisema.

Alisema kwa sasa wanachohakikisha ni kuona klabu zinapata asilimia 25 ya udhamini wao mapema ili zisaidie maandalizi ya timu na kuongeza kwamba wadhamini wakuu, Vodacom, nao watatoa fedha za nauli mapema tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

"Sasa tuko katika hatua za mwisho za mazungumzo na kampuni moja ambayo itakuwa ni wadhamini maalum wa kinywaji, kelele zisizo na msingi zinakimbiza watu wanaotaka kudhamini soka," aliongeza Karia.

Kama wataendelea kugomea, mechi 13 za ugenini za Yanga zitaonyeshwa kama kawaida kwavile si mali ya Yanga, ila 13 za nyumbani hazitaonyeshwa, hivyo klabu hiyo haitapata hata senti.

Mwenyekiti wa matawi wa Yanga mkoa wa Dar es Salaam, Bakili Makele, akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema kwamba hawataki kuona mechi zao za nyumbani na ugenini zinaonyeshwa na kampuni hiyo ya Azam Media mpaka pale watakapokaa tena mezani na kujadiliana upya kuhusu udhamini huo.

Makele alisema kwamba wakiacha udhamini wa sasa uliokubaliwa uanze kutumika ni sawa na kuwasaidia kiuchumi wapinzani wao ili wawazidi katika maendeleo ya soka.

"Msitulazimishe, tunamuomba Tenga (Leodegar - Rais wa TFF) akae na kupitia upya huo udhamini," alisema Makele.

TFF iliingia mkataba wa miaka mitatu na Azam Media wenye thamani ya Sh. bilioni 5.56 ambapo kila klabu itapata Sh. milioni 100 kwa msimu.

CHANZO: NIPASHE

0 comments: