CCM yamvua uanachama shemejiye Rais Karume

  Ni Mwakilishi na waziri wa zamani
Mwakilishi wa Kiembe Samaki (CCM) visiwani Zanzibar, Mansour Yussuf Himid.
Mwakilishi wa Kiembe Samaki (CCM) visiwani Zanzibar, Mansour Yussuf Himid, ambaye pia ni waziri wa zamani mwandamizi chini ya utawala wa Rais Amani Abeid Karume, amevuliwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mansour anayeelezwa kuwa ni shemeji yake na Rais Mstaafu Karume, alivuliwa uanachama huo na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM baada ya kusikiliza na kuridhia tuhuma dhidi yake kama zilivyokuwa zimekwisha kuamulia na Kamati Kuu Maalum ya Zanzibar iliyokaa chini ya Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Ali Mohamed Shein, Agosti 16, mwaka huu.

Mansour anafikwa na masahibu hayo huku akielezwa kuwa yuko nyuma ya kikundi cha Uamsho kilichoanzishwa Zanzibar hivi karibuni na kuleta mzozo mkubwa wa kisiasa na kijamii.

Jana Katibu wa Nec wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa Mansour ametiwa hatiani kwa tuhuma kadhaa ikiwamo kukisaliti chama chake.

Kwa maana hiyo, jimbo la uchaguzi la Kiembe Samaki sasa litakuwa wazi kwani maamuzi hayo yanamfanya Mansoor kupoteza ujumbe wa baraza la wawalikishi.

Halmashauri hiyo pia imeridhia kung’olewa kwa makatibu wa jumuiya za chama hicho akiwamo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM), Martine Shigela.

Maamuzi hayo ya NEC ni utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.

Nape alisema Mansoor amevuliwa uanachama kutokana na tuhuma za kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.

Alitaja tuhuma ambazo Nec imejiridhisha nazo vya kutosha ni kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.

Nape alitaja tuhuma nyingine ni kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM.

Tuhuma nyingine ni kuikana Ilani ya CCM ya uchaguzi Mkuu wa CCM wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM.

“Kwa uamuzi huo wa kumvua uanachama wa CCM kwa hiyo siyo tena mwanachama na wala kiongozi wa chama cha Mapinduzi,” alisema.

Alisema kuwa Mansoor hawezi kukata rufaa kwa sababu hicho ni kikao cha mwisho kikatiba kwa kutoa maamuzi yanayohusiana na chama.

Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansour zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 16, 2013 katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambapo wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama mwakilishi huyo.

Alidaiwa kushindwa kusimamia malengo, madhumuni na masharti ya chama.Aidha anadaiwa kutokusimamia wajibu wa mwanachama kwa kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM, kwa kukiuka Ilani ya chama hicho ya mwaka 2010.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa suala la kufukuzwa uanachama kwa mwakilishi huyo lilizua mjadala mzito katika kikao hicho, lakini baadaye wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kufukuzwa kwake.

Mansoor amekuwa miongoni mwa Wazanzibari walio katika safu ya mbele kutetea muundo wa Muungano utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.

MANSOUR NI NANI HASA
Mansour aliteuliwa kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi na Rais Karume mwaka 2000 na kuteuliwa kushika wadhifa wa Naibu Waziri wa Maji, Nishati Ujenzi na Ardhi hadi mwaka 2005.

Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki kupitia CCM, nafasi ambayo amedumu nayo hadi sasa. Mwaka huo aliteuliwa na Rais Karume kuwa Waziri wa Maji, Nishati Ujenzi na Ardhi hadi mwaka 2010.

Kati ya 2005 -2010 alikuwa Mweka Hazina wa CCM Zanzibar  wadhifa ulimpa fursa ya kuwa Mjumbe wa NEC na Kamati Kuu ya CCM. Mwaka 2010 hadi mwaka 2012, alikuwa Waziri wa Kilimo na Rasilimali.

Ilipofika 2009 alikuwa mstari wa mbele kuushutumu Muungano kuwa ni chanzo cha kudorora kwa Zanzibar huku akiendesha kampeni juu ya suala la mafuta kutokuwa la Muungano.
Katika uchaguzi wa mwaka jana ndani ya CCM, Mansour hakugombea nafasi yoyote ndani ya CCM.

Aidha, alihudumu kama mjumbe wa Baraza la Biashara la Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi 2012.

Kutokana na misimamo yake ndani na nje ya chama na Serikali, Oktoba 15, 2012, Dk. Shein ilifuta uteuzi wa Mansour kama waziri hivyo kubakia kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi hadi jana.

Mansour ni mwanasiasa na mfanyabiashara aliyezaliwa Novemba 3, 1967 kisiwani Unguja. Alisoma masomo yake ya msingi na sekondari nchini India kati ya mwaka 1976 na 1987.

Kabla ya kuingia rasmi katika siasa mwaka 2000, aliteuliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Wawakilishi na alijihusisha katika biashara ya hoteli.

Mwanasiasa huyo ni mtoto wa Mkuu wa Kwanza wa Jeshi la Zanzibar baada ya Mapinduzi, Brigedia Jenerali Yussuf Himid.

Amekuwa akisimamia maridhiano ya Wazanzibari na Umoja wa Kitaifa akiwa mmoja wa wajumbe sita wa Kamati ya Maridhiano aliyoshiriki kikamilifu kuyaanzisha mwaka 2009.

Pia ni miongoni mwa Wazanzibari walio mstari wa mbele kutetea muundo wa Muungano, utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.

Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Mwenyekiti Hassan Nassor Moyo (CCM), Eddie Riyami (CCM), Abubakar Khamis Bakari (CUF), Ismail Jussa Ladhu (CUF) na Salim Bimani (CUF).

Katika hatua nyingine Nec iliyokaa kwa siku tatu mjini Dodoma chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, pia kimeridhia uteuzi wa makatibu wa wapya wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Katika uteuzi huo aliyekuwa Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, nafasi  iliyokuwa ikishikiliwa na Shigela.

Taarifa za zaidi kutoka Dodoma ambazo zimelifikia gazeti hili jana jioni, zinasema kwamba Seif Shabani Mohamed ambaye ni mjumbe wa NEC kutoka Pemba ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Hamis Suleiman Dadi huku Amina Makilagi akiachwa kuendelea na nafasi yake ya Katibu Mkuu UWT.

Pia, NEC imeridhia mapendekezo ya CC ya kuziba nafasi za Makatibu wa CCM wa mikoa ya Morogoro, Kaskazini Pemba na Geita ambayo yamekuwa wazi kwa muda mrefu sasa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

Kutokana na hali hiyo, Romuli Rojas John ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro. John kabla ya uteuzi huo alikuwa Msaidizi Kitengo cha Uchaguzi, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM.

Aidha, Katibu wa CCM wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Kassim Mabrouk Mbarak, ameteuliwa kuwa Katibu mkoa Kaskazini Pemba wakati aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM mkoa wa Geita.

SAKATA LA MADIWANI BUKOBA

Kuhusu sakata la madiwani wanane wa Bukoba mjini waliotimuliwa na vikao vya CCM ngazi ya mkoa, Nape alisema kuwa suala hilo limeachwa kuendelea kushughulikiwa na kikao cha CC kilichokuwa kikiendelea jana usiku na kuahidi kutoa taarifa za maamuzi hayo leo.


Taarifa zaidi kutoka Dodoma zilieleza kuwa jana jioni baada ya NEC kumaliza kikao chake, wajumbe wa CC waliendelea kukutana na viongozi kadhaa wa CCM Mkoa wa Kagera akiwamo Mwenyekiti na Katibu wa Wilaya ya Bukoba.

Mapema jana kabla ya kikao cha NEC kuanza, Kamati Kuu ilikutana na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani na kuwahoji na baadaye kuwahoji Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa wa Kagera.

MSIMAMO WA CCM KUHUSU RASIMU YA KATIBA

Wakati Nape akiweka kiporo taarifa juu ya maamuzi yaliyofikiwa na Nec kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ahadi ya kutolewa baadaye, habari zinasema mambo matatu mazito ya rasimu hiyo yamekataliwa.

Habari ambazo NIPASHE ilizipata kutoka Dodoma zinaeleza kuwa Nec imekataa suala la kuweka kikomo cha vipindi vitatu kwa wabunge.  Badala yake imependekeza mfumo wa sasa wa bila ukomo kuendelee.

Aidha, chama hicho kimekataa pendekezo la mawaziri wasitokane na wabunge na kutaka utaratibu wa sasa wa mawaziri kutokana na wabunge uendelee.

Kuhusu mfumo wa Muungano wa serikali tatu, CCM imepinga pendekezo hilo na badala yake kutaka mfumo wa serikali mbili uendelee kama ulivyo sasa.

Pendekezo ya Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba ya kuwa na uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wabunge wanawake na wanaume limekubaliwa na chama hicho tawala.
CHANZO: THE GUARDIAN

0 comments: