RUFAA YA UBUNGE: Lissu aibuka kidedea


  Ajigamba: rufaa haikuwa na 'kichwa wala miguu'
Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema)
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ameibua kidedea katika shauri la rufaa iliyokatwa, dhidi ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu iliyomthibitisha ubunge wake.


Hatua hiyo inatokana na Mahakama ya Rufani Tanzania, kukubaliana na ombi la kuitupa
rufani ya kutengua hukumu ya awali, iliyotolewa na Mahakama Kuu

Mahakama hiyo pia imewaamuru warufani kulipa gharama zote zilizotumika kuendeshea kesi hiyo katika Mahakama Kuu na mrufani wa pili, kulipa gharama za kesi kwa upande wa Mahakama ya Rufani.
Warufani hao ni Shaban Selema na Pascal Halu ambao kwa nyakati tofauti, walijitoa kuendelea na kesi hiyo.

Uamuzi huo wa mahakama umefikiwa baada ya warufani wote kujitoa katika kesi hiyo namba 49/2013, ambayo ilisikilizwa na jopo la majaji Engela Kileo, Salumu Massati na Natalia Kimaro wa Mahakama hiyo.

Akisoma Hukumu hiyo, Jaji Kileo alisema kuwa mahakama hiyo imekubaliana na ombi la kuondoa rufani hiyo mahakamani kwa mujibu wa kanuni 4(a) na (d) za kanuni za mahakama ya mwaka 2009.

“Kwa mujibu wa Kanuni 4(a)(d) za kanuni za mahakama ya rufani mwaka 2009, tumekubali rufani hii iondolewe mahakamani,” alisema Jaji Kileo.
Aidha, alisema pamoja na kukubali ombi hilo pia mrufani wa pili Pascal Halu, atazilipa gharama zote za mahakama hiyo kutokana na kuchelewa kutoa taarifa ya kutoendelea na rufaa hiyo.

“Gharama za kesi zitalipwa na mrufani wa pili kwa upande wa Mahakama ya Rufani na katika Mahakama Kuu, gharama zitalipwa na wote wawili kama ilivyoamuriwa awali,” alisema Jaji huyo.

Awali, wakisikiliza kesi hiyo ambayo warufani hao waliwakilishwa na wakili aliyekuwa akiwatetea, Godfrey Wassonga, Jaji huyo alisema kuwa
mahakama hiyo haiwezi kuendelea na kesi ambayo warufani wamejitoa.

Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikisikilizwa kulionekana ushindani wa kisheria wa nani anapaswa kulipa gharama hizo ambapo Lissu aliyekuwa akijitetea mwenyewe, aliitaka mahakama hiyo kumuamuru
wakili aliyekuwa akiwatetea kulipa gharama zote za kesi hiyo.

Hata hivyo, Wassonga alidai kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachoeleza wakili anapaswa kulipa gharama hizo.

Baada ya mvutano huo majaji walidai kuwa notisi ya kuondolewa kesi hiyo ilichelewa wakati shauri hilo lilikuwa limepangwa kusikilizwa.

Jaji Engela alisema wakili huyo msomi wa utetezi, Wassonga, aliomba kuondolewa kwa rufani hiyo chini ya kifungu namba 102 cha kanuni za
mahakama ya rufani ya mwaka 2009.
“Mei, mwaka huu, Shaban aliwasilisha kiapo mahakamani akieleza hakutoa maelekezo kwa Wassonga kufungua rufani hiyo ambayo warufani ni Lissu,Vicent Tangoh ambaye ni wakili mkuu wa serikali pamoja na Killey Mwitasi,” alisema Jaji.

Alisema wameliangalia suala hilo kwa makini na katika hali ya kawaida notisi ya kutoa isingesikilizwa kabla ya shauri kutoka na kuchelewa.

Aidha alisema kuwa mrufani wa pili ambaye ni Halu alijitoa katika kesi hiyo kwa kuandika barua Septemba 7, mwaka huu pia alikuwa amechelewa, kwani tayari tarehe ya shauri hilo ilikuwa imepangwa, hivyo atalipa gharama za kesi hiyo.

LISSU: RUFAA ILIKUWA HAINA KICHWA WALA MIGUU
Akizungumza nje ya mahakama, Lissu alisema kuwa hukumu hiyo haijamshangaza kwa sababu rufaa hiyo `haina kichwa wala miguu’, kwani imeletwa na watu wasiojua sheria.

“Kwa hiyo sijashangaa hata kidogo kuwa Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali, nataka kusema tu kwamba huyo wakili wao ana bahati vinginevyo
alitakiwa kulipa hizo gharama mwenyewe,” alisema.

AMHUSISHA KINANA

Lissu alisema, “wakili analipwa na kina Kinana hata bila ya kuwaambia wahusika, yeye amefungua rufaa wakati tangu mwezi wa tano warufani wamemwambia kuwa hawataki kuendelea na kesi, lakini rufaa imeletwa kwa sababu tu
Kinana amesema.”
WASSONGA: NI HUKUMU YA KAWAIDA

Kwa upande wake, Wakili Wassonga, alisema hukumu hiyo ni ya kawaida na warufani hao watalipa gharama zote za kesi.

Aprili mwaka jana Mahakama Kuu ilimtangaza Lissu kuwa mshindi halali wa ubunge katika jimbo hilo. 
CHANZO: NIPASHE

0 comments: