Shein: Ni ukatili

 
  Padre Mwang`amba ahamishiwa Muhimbili
  Aliyemmwagia tindikali kupatikana kirahisi
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameitaka polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio ya watu kumwagiwa tindikali, ili wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Dk. Shein alitoa agizo hilo jana katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, alipokwenda kumjulia hali Padre Anselmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki, parokia ya Machui, aliyemwagiwa maji yanayosadikiwa kuwa tindikali, juzi jioni.
“Hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee...ni lazima jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Amekiita kitendo hicho kuwa ni cha kikatili na kisichovumilika na kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Dk. Shein, alielezea kusikitishwa na kitendo hicho na kumpa pole Padre Mwang’amba na kumuomba Mwenyezi Mungu ampe nafuu haraka apone ili aendelee kuitumikia jamii.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo nje ya wodi hiyo, Dk. Shein, aliwataka waumini hao kuwa na subira wakati serikali ikichukua hatua kukabiliana na kitendo hicho.
“Ni jambo la kusikitisha kumfikisha binadamu mwenzako katika hali kama hii ya majonzi. Hakuna anayeyataka haya. Tuwe wastamilivu serikali tunachukua hatua,” aliwaambia waumini hao.
Akizungumzia hali yake, Padre Mwang’amba alimueleza Rais kuwa ni nzuri, lakini anatarajia kupata nafuu zaidi baada ya uvimbe kupungua sehemu za machoni.
“Hali yangu ni nzuri lakini natarajia uvimbe ukipungua nitaona vizuri zaidi” alisema Padri Mwang’amba na kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake hakuathirika sana.
Alisema tukio hilo lilitokea eneo la Mlandege jioni, wakati akitoka katika ofisi moja inayotoa huduma za `intaneti’ katika eneo hilo ndipo akatokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mohamed Saleh Jidawi, akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Jamala Adam Taibu, amesema alipofikishwa katika hospitali hiyo, Padre Mwang’amba alipatiwa huduma zote muhimu .
Kuhusu majeraha aliyopata, Dk. Jidawi alisema kuwa kwa ujumla asilimia 30 ya mwili wake (Padre Mwang’amba) umeathirika na kidogo sehemu za macho.
Padre Mwang'amba, amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Padre Mwang'amba alifikishwa hospitalini hapo majira ya saa 4:00 asubuhi akitokea Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.
Alisafirishwa kwa ndege iliyokodiwa na Kanisa Katoliki nchini, ambapo aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere majira ya saa 3.30 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja kwenye wodi ya wagonjwa wa dharura kwa ajili ya uchunguzi.
Akizungumza mara baada ya kufikishwa wodi namba 10 jengo la Kibasila, Padre Mwang'amba alisema hali yake inaendelea vizuri, madaktari wanaendelea kumpatia tiba. "Nashukuru hali yangu inakwenda vizuri, nimewasili leo (jana) madaktari wanaendelea kunitibu," alisema.
Hata hivyo, hakutaka kuongeza zaidi na kuomba aachwe ili apumzike.
Mkuu wa wauguzi wa jengo hilo, Ruthi Rutabingwa, alisema amempokea mgonjwa huyo na jitihada za kitabibu zinaendelea kufanywa.
"Nathibitisha kumpokea mgonjwa akiwa katika hali ya kuridhisha," alisema Rutabingwa.
Katika hatua nyingine, mmoja wa watu walioambatana naye kutoka Zanzibar, ambaye hakutaja jina lake litajwe, alisema mtu aliyefanya tukio hilo anaweza kujulikana haraka kutokana na nyumba aliyokimbilia kujificha kufahamika.
Alisema, mtu aliyemmwagia tindikali kiongozi huyo wa kidini, mara baada ya tukio hilo alikimbilia kwenye nyumba moja jirani na eneo hilo na baadhi ya watu walimuona.
"Kama polisi itakuwa makini, kazi ya kumpata yule kijana itakuwa rahisi kwa sababu baada ya kummwagia padre tindikali alikimbilia kwenye nyumba moja," alisema.
Alisema wakati wanakuja Dar es Salaam, amesikia watu wanaoishi kwenye nyumba hiyo wamekamatwa kwa mahojiano. 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment: