Maandamano yatikisa Dodoma

Maelfu ya wakazi wa Kata za Kikuyu Kusini na Kilimani katika Manispaa ya Dodoma, wameandamana kupinga amri iliyotolewa na Mamlaka ya Ustawishaji ya Makao Makuu (CDA) ambayo inawataka kuhama katika eneo hilo ndani ya siku saba.



Wakazi hao waliandamana jana kutoka Kikuyu hadi Viwanja vya Nyerere Square katikati ya Manispaa ya Dodoma wakimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, kuzungumza nao ili kuwaeleza hatima ya nyumba zao 1,000 kubomolewa kwa madai ya kulivamia eneo la CDA.

Maandamano hayo yalisindikizwa na ulinzi wa polisi hadi katika viwanja hivyo huku wakazi hao wakiwa wameshikilia mabango yenye ujumbe mbalimbali wakupinga hatua hiyo.

Wakazi hao wakiwa wanaimba nyimbo mbalimbali huku wakiinua mabango yao juu yenye ujumbe kama “CDA ni zaidi ya al Shaabab”, “CCM mnaiona bomoabomoa”, “CDA ni zaidi ya Nduli Idd Amini Dada” na lingine likisomeka “hata wanyama hupewa hifadhi.”

Wakizungumza na waandishi wa habari katika viwanja hivyo wakati wakimsubiri Dk. Nchimbi, baadhi ya wananchi na viongozi wao wa mitaa walidai kuwa lengo la maandamano hayo ni kufikisha kilio chao kwa serikali ya mkoa.

Andrew Mdumi, mMenyekiti wa Mtaa wa Mkalama ambao ni sehemu ya eneo linalotakiwa kuvunjwa, alisema waliamua kufanya maandamano hayo baada ya kupewa amri ya kuondoka katika eneo wanaloishi kwa kipindi kirefu.

Mdumi alisema kuwa CDA imekuwa ikiwapatia namba kila wakati na kuwaahidi kuwa wataalamu wake wa ardhi watakwenda kuwapimia, lakini katika hali ya kushangaza imewapa amri ya kuondoka ndani ya siku saba kuanzia Septemba 23, mwaka huu kwa madai kuwa wamevamia katika eneo hilo ambalo lilikuwa limetengwa kwa ajili ya bustani za mbogamboga na matunda.

“Wanataka tuondoke ili kupisha kilimo cha mbogamboga na matunda, hivi kweli mboga na maisha yetu kipi cha msingi, kuna nyumba zaidi ya 1,000 ambazo wanataka kuzibomoa kwa ajili tu ya kupisha bustani,” alisema.

Alisema wakazi hao wamekuwa wakishirikiana na CDA kwa kipindi kirefu ili kufanikisha zoezi la upimaji wa viwanja hivyo kwa gharama zao wenyewe.

Mwenyekiti wa kamati ya upimaji katika Kata ya Kikuyu Kusini, Mathew Ndallu, alisema kuwa katika kufuatilia kupimiwa viwanja, walikutana na CDA na kukubaliana kuwa waende kufanya utambuzi wa nyumba zilizopo Mapagale na Misingi ili ufanyike upimaji.

 Ndallu alisema walikubaliana kuwa kwa eneo hilo kuwa halijapimwa, wako tayari kuchangia gharama za upimaji ili kuwezesha zoezi hilo kufanyika.

“Tulikubaliana nao baada ya wao (CDA) kuja kutambua idadi ya nyumba Mapagale na Misingi watupimie na sisi tuko tayari kuchangia kiasi cha Shilingi 500,000 kwa kila mwenye eneo,” alisema Ndalllu.

 Aliongeza kuwa baada ya CDA kuonekana kutoridhika na kiasi hicho, wananchi  walisema watakuwa tayari kuongeza Sh. 200,000 ili gharama za kupimiwa zifikie Sh. 700,000.

Hata hivyo, alisema katika hali ya kushangaza wakati wakisubiri kupimiwa, CDA iliwageuka na kuwataka kwanza wapatiwe viwanja 500 ili wawapimie.

“Mara baada ya kukubaliana nao kuwa tuko tayari kuchangia, Mkurugenzi alituambia kwanza tuwape wao viwanja 500 ili waje kutupimia na kama hatutakubali basi watakuja kutubomolea,” alisema Ndallu.

Alisema baada ya wao kukataa kumpa mkurugenzi huyo viwanja hivyo, aliwaandikia barua hiyo ambayo ilikuwa inawataka wakazi wa maeneo hayo kuondoka kabla ya jana ili leo zoezi la kubomoa nyumba zao lianze.

“Walituandikia barua ambayo inatutaka kuaondoka ndani ya siku hizo saba ikiwa ni kuanzia tarehe 23 ya mwezi huu ambapo inaishia leo (jana) na kesho (leo )wanakuja kuanza kubomoa” alisema Ndallu.
 Alisema kutokana na CDA kushindwa kusikiliza kilio chao, wameona kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya wao kupata suluhu ya tatizo lao.

Alisema kuwa jumla ya mitaa minne katika kata hizo ndiyo inayotakiwa kubomolewa ambayo ni mitaa ya Mkalama, Chidachi na Image A na B.

RC ATENGUA AMRI
Akizungumza na kundi la wakazi hao, Dk. Nchimbi alisema kuwa anatengua amri hiyo iliyotolewa na CDA na kumtaka Mkurugenzi wa mamlaka hiyo kukutana na viongozi wa maeneo husika kwa ajili ya mazungumzo ya kupata mwafaka.

“Naitengua amri hiyo na namwagiza Mkurugenzi akutane na wananchi hawa pamoja na viongozi wao ili kufikia mwafaka kwani kubomoa siyo suluhu, hamuwezi kubomoa Dodoma nzima na ningependa kuletewa taarifa juu ya suala hili,” alisema Dk. Nchimbi na kuongeza:

“Mnachotakiwa ni kuboresha na kutumia njia sahihi ambazo hazitawaumiza wananchi ambao ndiyo wateja wenu.”

Baada ya Mkuu wa mkoa kutamka kutengua amri hiyo, wananchi hao walipaza sauti kwa furaha huku wengine wakisema wanamuombea kiongozi huyo miaka 20 zaidi ya uongozi kama mkuu wa mkoa na ikiwezekana astaafie kazi mkoani Dodoma.

CDA: BOMOABOMOA PALE PALE
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskas Muragili, hata hivyo, baadaye aliliambia NIPASHE kuwa  agizo la mkuu wa mkoa hajalipata kimaandishi, hivyo zoezi la kubomoa nyumba hizo liko pale pale kwa kuwa CDA ilishatoa notisi ya siku saba kwa wamiliki wa nyumba hizo kuzibomoa wenyewe.
Alisema kuwa CDA ni mamlaka inayojisimamia na kuongozwa na sheria.

CHANZO: NIPASHE

0 comments: