Sumaye aanza `vita` yawazi dhidi ya Lowassa
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
Sumaye jana aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kumwandama Lowassa kwa maelezo kuwa anausaka urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa kutumia mbinu tofauti ikiwamo za kuupotosha umma kuhusu kile alichokiita kuwa ni ‘ukweli kuhusu mradi wa maji yanayotoka kwenye Ziwa Viktoria’.
Septemba Mosi mwaka huu, Lowassa alikaririwa na vyombo vya habari, akielezea jinsi mradi wa kuvuta maji kutoka Ziwa Viktoria ulivyopingwa na wajumbe wa baraza la mawaziri la utawala wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Alisema mawaziri wawili pekee (kwa wakati huo) Jakaya Kikwete (Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) na Mohamed Seif Khatibu (Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais), walimuunga mkono kuhusu mradi huo unaoinufaisha mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sumaye alisema kauli ya Lowassa inaupotosha umma na kwamba mradi huo ulipata idhini ya mawaziri wote akiwamo yeye (Sumaye) wakati huo akiwa Waziri Mkuu.
“Sipendi kuzungumzia mambo ya watu, lakini pale inapoonekana kuna upotoshaji wenye kuiathiri jamii, siwezi kunyamaza kimya kwa maana hapa ni kama ametukanyaga vidole sisi tuliokuwa kwenye baraza hilo,” alisema Sumaye.
Pamoja na kumtumia maneno makali dhidi ya Lowassa kwa kile alichokiita kuwa ni ‘uongo mkavu’, Sumaye alisema kutoa siri za baraza hilo ni kosa la jinai ambalo mhusika wake anastahili kufungwa jela.
“Labda alizungumza kwa sababu alijua kwamba siyo taarifa za kweli, hivyo hawezi kushtakiwa, lakini kutoa siri za baraza la mawaziri ni kosa la jinai,” alisema.
UHALISIA WA MRADI
Sumaye alisema mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria ni wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukiasisiwa na Rais wa wakati huo, Mkapa.
Kwa mujibu wa Sumaye, maji ya Ziwa Viktoria yaliwekewa vikwazo vya makubaliano ya kati ya 1952/53, yaliyozizuia nchi kama Tanzania, Kenya na Uganda kuyatumia, ili kuyanusuru mataifa ya Misri na Sudan yasiathirike.
Sumaye alisema hatua za awali katika kufanikisha mradi wa maji ya ziwa hilo, zilifanyika wakati Waziri wa Maji akiwa Dk. Pius Ng’wandu na baadaye Mussa Nkhangaa, ingawa ukamilifu wake ukatimia wakati Lowassa akiwa Waziri mwenye dhamana.
Alisema hata yeye (Sumaye) alishiriki kwa namna tofauti kufanikisha mradi huo, huku akisisitiza kwamba kauli njema kuhusu ufanisi wake zinapaswa kuelekezwa kwa serikali ya Mkapa na CCM badala ya mtu binafsi.
“Kwa hiyo mtaona kwamba wakati wa hatua za awali za mradi huo, Lowassa hakuwa Waziri wa Maji, yeye aliteuliwa wakati umeshaiva na alichokifanya kingefanywa na yeyote ambaye angeteuliwa kushika wadhifa huo kwa sababu ulikuwa wa serikali,” alisema.
Sumaye alisema kasi ya kufanikisha mradi huo ilichochewa na hali ya ukame iliyokuwa imeuathiri mkoa wa Shinyanga kiasi cha kusababisha baadhi ya wakazi wake kuhama, hivyo kumfanya Mkapa (akiwa rais) kuapa kwamba mradi huo ungetekelezwa kwa gharama zozote.
Alihoji: “Kama mawaziri wengine wangekataa isingewezekana kwa Waziri mmoja kutekeleza mradi, angetoa wapi fedha za mradi huo?”
AMBEZA LOWASSA
Sumaye alisema katika hali inayoonesha kuwa mradi huo ulikuwa ‘mikononi’ mwa baraza la mawaziri la Mkapa, Lowassa hakutekeleza hatua yoyote hata alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu chini ya Rais Jakaya Kikwete.
“Kama aliyoyasema ni sahihi, baada ya kuwa Waziri Mkuu, ameshindwa vipi kuyafanya maji ya Ziwa ya Viktoria kufika hadi Dodoma, badala yake yameishia pale yalipofikishwa wakati wa utawala wa Mkapa?” alihoji.
“Anayestahili heshima kwa mradi ni Mzee Mkapa, sasa sisi wanasiasa tusipende kuwapa watu utamu wa ukweli unaopakwa juu wakati ndani ni machungu ya uongo,” alisema bila kufafanua.
LOWASSA: NINAMHESHIMU, SIHITAJI MALUMBANO
Lowassa akizungumza na NIPASHE kupitia kwa mmoja wa wasaidizi wake, Aboubakar Liongo, alisema hawezi kujibizana na Sumaye, kiongozi aliyewahi kushika wadhifa wa juu katika utumsihi wa umma (Waziri Mkuu).
“Amesema hawezi kumjibu Sumaye kwa maana hakufundishwa hivyo katika maadili ya utumishi wa umma,” alisema Liongo.
Hata hivyo, Liongo alisema Lowassa katika tukio lililohusishwa na Sumaye, hakutamka kwamba ufanisi wa mradi huo ulitokana na yeye (Lowassa), isipokuwa alikuta wakazi wa Shinyanga wakiwa wanauita mradi huo kwa jina lake (Lowassa).
KUJIWEKA KANDO NA MAFISADI WA CCM
Wakati huo huo, Sumaye amesema ikiwa CCM itapitisha majina ya watuhumiwa wa rushwa na ufisadi kuwania nafasi za uongozi na uwakilishi katika uchaguzi mkuu wa 2015, hawezi kushirikiano nao hata kama atabaki ndani ya chama hicho.
Sumaye aliunga mkono angalizo lililotolewa na Rais Kikwete hivi karibuni, kuwa kama rushwa itazidi ‘kuweka makazi yake ndani ya CCM’, chama hicho kitashindwa katika uchaguzi mkuu huo.
ASHAURI TANZANIA ISIJITOE EAC
Sumaye alizungumzia pia mzozo unaojitokeza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Tanzania ikilalamikia kutengwa na nchi za Uganda, Kenya na Rwanda na kusema, wazo la kujiondoa katika jumuiya hiyo si sahihi.
Alisema msingi wa makubaliano yaliyofikiwa katika kuanzishwa upya kwa EAC, ulilenga kuifanya jumuiya hiyo kuwa yenye maslahi na manufaa kwa wananchi, wakiwa na dhamana ya kuukubali ushirikiano huo ama vinginevyo.
Alisema hali ilivyo sasa ambayo viongozi wakuu wa nchi wanaonekana kuteka nyara haki na ushiriki wa umma kuamua hatima ya EAC, haipaswi kuendelea.
MABILIONI YA FEDHA YALIYOFICHWA USWIZI
Sumaye alisema umefika wakati kwa serikali kushirikiana na nchi za nje ili kuwabaini viongozi wa umma walioficha fedha nje, ikibidi zitaifishwe na kurejeshwa nchini.
Alisema tangu akiwa Waziri Mkuu hata sasa, hajawahi kufungua na kumiliki akaunti ya benki ya nje ya Tanzania, ingawa alithibitisha kupata shinikizo kutoka kwa mawaziri wa serikali (hakuwataja majina) ili afanye hivyo.
“Kuna wakati mawaziri walinishangaa kwa nini Waziri Mkuu (wakati huo) sina akaunti nje ya nchi … sasa mimi pia ninauliza kwa nini serikali isilete orodha ya wahusika badala ya kuliacha suala hili kuwa jumla,” alihoji.
KUFUNGIWA MAGAZETI
Sumaye alisema hulka ya kuviadhibu vyombo vya habari ikiwamo kuyafungia magazeti, kunapaswa kufanywa kwa makosa makubwa kama uchochezi wa jeshi ili liasi dhidi ya serikali ama mafarakano dhidi ya nchi jirani.
“Lakini kama kosa ni dogo linalozungumzika, ni muhimu watawala wakakutana na wahusika na kuzungumza, kwa maana huwezi kuongoza nchi ukitegemea umma unaoungoza usikusema ikibidi kupitia vyombo vya habari,” alisema.
URAIS 2015
Sumaye alisema ni mapema kutamka nia yake ya kuwania ama kutowania urais katika uchaguzi mkuu wa 2015, kwa vile CCM ambayo yeye ni mwanachama wake, ilishapiga marufuku kufanya hivyo.
Hata hivyo, Sumaye alisema anaamini kuwa ana haki na uwezo wa kuwania urais kwa vile umma wa Watanzania unamkubali na anazungumzika kwa jamii, kwamba anafaa kwa nafasi hiyo.
Ingawa Sumaye anatamba kuungwa mkono na umma katika uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kupitia wilaya ya Hangang mwaka jana, alidondoshwa na mpinzani wake, Dk. Mary Nagu ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji).
UZINDUZI WA MRADI
Uzinduzi wa mradi huo ulifanyika Januari, 2009 na Rais Jakaya Kikwete alimsifia mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, kwa uthubutu wake katika mradi huo ambao awali ulipangwa kukamilika 2010.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments: