Mnyaa ataka bunge livunjwe

Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, ameshauri Mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba unaoendelea uahirishwe kwa mwezi mmoja au miwili.


Amesema hilo litasaidia kuepusha uvunjifu wa amani unaoweza kutokea nchini kutokana na mivutano iliyokithiri ndani ya Bunge hilo, ambayo hatima yake haitabiriki.

Alisema hayo alipozungumza katika mahojiano maalumu na NIPASHE katika viwanja vya Bunge, mjini hapa jana.

Alisema kutokana na hali inayoendelea hivi sasa katika Bunge hilo, linatakiwa liahirishwe na kulipisha lile la Bajeti liendelee na vikao vyake.

Mnyaa alisema baada ya Bunge hilo kuahirishwa uandaliwe utaratibu wa kura ya maoni, ambayo wananchi watapewa fursa ya kuulizwa waamue muundo wa Muungano wanaoutaka.

“Kama wananchi wataamua muundo wa serikali tatu, basi Rasimu ya Katiba ipite. Na kama wataamua serikali mbili, basi rasimu hiyo iondolewe,” alisema Mnyaa.

Alisema vinginevyo, kinachoendelea hivi sasa ni kupoteza bure fedha za wananchi, ambazo zingetumika katika kushughulikia vipaumbele vingine vya kitaifa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: