Klabu 13 zaipinga Yanga

Klabu 13 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana zilitoa tamko la kuunga mkono udhamini wa kampuni ya Azam Media katika ligi hiyo na kupinga hatua ya Yanga kukataa udhamini huo unaotarajiwa kudumu kwa muda wa miaka mitatu.

Akizungumza kwa niaba ya klabu hizo jana kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba wameamua kuungana na kutoa msimamo wao kufuatia kauli iliyotolewa na Yanga hivi karibuni ambapo walieleza kuwa udhamini wa Azam Media umekuja kuokoa soka la Tanzania.

Kamwaga alisema kuwa kwa muda mrefu klabu zilikuwa zinaomba kampuni mbalimbali zijitokeze kudhamini ligi hiyo na baada ya Azam Media kuamua kudhamini ligi wameipongeza na kusema kuwa kilio chao cha muda mrefu kimeanza kupata ufumbuzi.

Alisema kwamba udhamini wa Azam Media utasaidia kuziongezea klabu fedha kutoka Sh. milioni 70 kwa msimu hadi kufikia Sh. milioni 170 na kuizidi Ligi Kuu ya Kenya ambapo klabu zinatapa Sh. milioni saba za Kenya ( sawa na Sh. milioni 125 za Tanzania) kwa mwaka.

"Udhamini wa SuperSport ambao unaliliwa na baadhi yetu ni mdogo zaidi ukilinganisha na dola milioni moja ambazo Azam Media wa hapa nchini amekubali kutoa kwa mwaka... ni imani yetu kwamba udhamini huu utaifanya ligi ya Tanzania kuwa bora kuliko zote Afrika Mashariki," alisema Kamwaga.

Alieleza pia kwa mujibu wa katiba za FIFA, CAF na TFF, haki za televisheni zipo chini ya shirikisho hilo na klabu zote 14 zilishirikishwa katika mchakato wa kumpata mdhamini huyo.

Aliongeza kuwa hoja ya Yanga kukataa udhamini huo kwamba bodi iliyojadili na kuikubali Azam Media haina nguvu kisheria kwa sababu ni ya mpito haina mashiko kwa sababu TFF ndiyo iliyoiungia mkataba na wadhamini hao na si Kamati ya Ligi kama inavyojulikana kwa sasa.

Alimtaja Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga na katibu wao, Lawrence Mwalusako, kuwa ndiyo walikuwa wakihudhuria vikao na kushangazwa kauli za kuingiwa na hofu ya kuhujumiwa kwa klabu yao kwa sababu tu wadhamini hao wanamiliki timu ya Azam ambayo pia inashiriki ligi na imeonyesha upinzani kwa klabu kongwe za soka nchini.

Pia wanashangazwa na hoja ya Yanga kutaka wapewe mgawo mkubwa zaidi ya klabu nyingine wakati kanuni zinaeleza kwamba fedha zinakazopatikana zitagawiwa sawa sawa.

"Kama ilivyokuwa kwa Vodacom, fedha za milangoni, GTV na Star TV, udhamini huu pia utafuata mfumo ule ule," aliongeza.


Alisema pia kuhusiana na suala la mapato ya milangoni kupungua endapo mechi zitaonyeshwa kwenye televisheni 'live' jambo hilo si sahihi kwa sababu rekodi zinaonyesha mechi zote kubwa iliyoonyeshwa ndiyo iliyoingiza mapato ya juu zikiwamo mechi za watani na za timu ya taifa ya Tanzania (Stars vs Ivory Coast).

"Tunawashauri wenzetu wa Yanga waanze kuamini kwenye kitu kinachoitwa Uwajibikaji wa Pamoja. Mambo yanayoamuliwa kwenye vikao hayapaswi kupingwa nje ya vikao," aliongeza.

Naye Mkurugenzi wa Kagera Sugar, Ahmed Yahaya, alisema kuwa hakukuwa na siri katika mchakato wa kuipa Azam Media haki ya kuonyesha mechi za ligi kwenye televisheni kama inavyodaiwa na Yanga.
Alisema pia tangu udhamini huo ulipotangazwa hakuna kampuni nyingine iliyojitokeza na kutoa dau la juu zaidi ya Azam Media na endapo atapatikana watakaa upya na kujadili ofa.

Klabu hizo zinazoipinga Yanga ni pamoja na Simba, Azam , Ashanti United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, Mgambo JKT, JKT Oljoro, Rhino Rangers, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Kagera Sugar.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: