Sitta: Ninachonganishwa na wabunge wa CCM

Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), Samuel Sitta, amesema mahasimu wake kisiasa, wameimarisha mkakati wa kumchonganisha na wabunge, ili kufifisha jitihada zake za kupambana na ufisadi.

Sitta amesema mahasimu hao ambao hata hivyo hakuwataja majina, wameanza kutumia baadhi ya vyombo vya habari, kuiaminisha jamii jamii kwamba, anawakosoa wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Viti Maalum.

Hivi karibuni, Sitta alikaririwa na gazeti moja la kila siku (sio Nipashe), akidai baadhi ya wabunge ni mzigo huku wale wa viti maalum wakiwa hawana umuhimu katika taasisi hiyo ya uwakilishi wa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari jimboni jana, Sitta alisema taarifa hizo ni mwendelezo wa upotashaji wa kauli anazozitoa, lengo likiwa na kumwathiri katika vita dhidi ya ufisadi.

“Nimebaini kuwa upotoshwaji huo ni sehemu ya mkakati wa kundi la kisiasa ambalo kinara wake anautafuta Urais wa nchi kwa udi na uvumba huku akibebwa na marafiki matajiri,” alisema.

Alitoa mfano kuwa, alipokuwa Busega hivi karibuni, alitoa wito kwa wabunge wenzake wa CCM, kuyatangaza mafanikio ya utendaji wa serikali ya CCM katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Alisisitiza umuhimu kwa wabunge hao kutembelea majimbo yao na kuelezea mafanikio katika maeneo kama ujenzi wa barabara, usambazaji umeme na huduma za jamii.

Kuhusu wabunge wa viti maalum, Sitta alisema chanzo cha upotoshaji uliofanyika ni kauli yake ya kuunga mkono mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwamba wanawake na wanaume wagombee ubunge kwa kuchaguliwa sawia katika majimbo.

“Nilieleza kuwa utaratibu huo utawajengea wanawake uzoefu wa kugombea nafasi kwa mchujo unaotokana na mikutano ya hadhara.  Pili kwa kuchaguliwa majimboni, wanawake nao watawajibika moja kwa moja kwa wananchi kuliko ilivyo hivi sasa katika utaratibu wa viti maalum,” alisema.

Alisema, anatambua na ataendelea kutambua mchango wa wanawake kwa taifa, na kutoa mfano kuwa hatua inathibitika kwa jinsi aliasisi mabadiliko yaliyosababisha kuongeza uwakilishi wa wanawake katika Bunge, alipokuwa Spika.

“Isitoshe hata mke wangu ni Mbunge wa viti maalum na ni kielelezo cha jinsi wanawake wanavyoweza kufanya vizuri pale wanaume tunapowaunga mkono,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: