Yanga mwendo mdundo ikiua Azam

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik akimkabidhi ngao ya Jamii kwa kapteni wa timu ya Yanga Nadir Haroub `Cannavaro.`( Picha na Khalfan Said)
Licha ya kulazimika kubadili wachezaji wawili kutokana na majeraha katika nusu saa ya kwanza ya mchezo, Yanga jana ilitwaa taji la kwanza kati ya manne inayoshindania msimu huu, ilipoilaza Azam 1-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii, kwenye Uwanja wa Taifa.
Ikizua hofu kwa mashabiki wake ya kushindwa kuendelea pale ilipotwalia ubingwa wa Bara msimu uliopita, nafasi ya Aly Mustafa ilichukuliwa na Deogratias Munishi katika dakika ya 26 baada ya mlinda mlango huyo kuumia akijaribu kumzuia John Bocco wa Azam asifunge.
Wakati huo, kocha wa Yanga Ernie Brandts alikuwa ameshalazimika kumuingiza kiraka Mbuyu Twite kuchukua nafasi ya beki Kelvin Yondani dakika 10 kabla ya kipa huyo, kutokana na sababu hiyo hiyo dhidi ya mshambuliaji huyohuyo wa Azam.
Iliichukua Yanga inayowania pia ubingwa wa Bara, Kombe la Kagame la Afrika Mashariki na Kati na taji la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu dakika mbili tu kupata bao lililoipa Ngao ya Jamii.
Bao hilo lilifungwa na Salum Telela kwa shuti baada ya mabeki wa Azam kutomkaba wakidhani angeusambaza, mfungaji akiwa alipata pasi kutoka kwa mshambuliaji wa Burundi Didier Kavumbagu.
Khamis Mcha aliipotezea Azam iliyoshika nafasi ya pili msimu uliopita nafasi nzuri ya kusawazisha katikati ya kipindi cha kwanza, baada ya shuti lake kuokolewa na Nadir Haroub huku lango likiwa wazi kutokana na Mustafa kuwa alishaanguka chini langoni mwa Yanga.
Kabla ya Mcha kupoteza nafasi hiyo, mshambuliaji hatari wa Azam Boco alikuwa ametoka kushindwa kufunga bao rahisi baada ya Mustafa kuokoa mpira miguuni mwake dakika nane tangu bao la Yanga.
Kumalizika kwa pambano la Ngao ya Jamii ni ishara kuwa pazia la msimu mpya wa ligi kuu ya Bara limefunguliwa na sasa Yanga itakuwa mwenyeji wa timu iliyopanda tena daraja ya Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi miongoni mwa mechi saba.
Azam itacheza ugenini Manungu Complex na Mtibwa Sugar siku hiyo pia wakati JKT Oljoro na Coastal Union zitakuwa kwenye Uwanja wa Sherikh Amri Abeid na Mgambo JKT na JKT Ruvu zitapambana kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Timu mpya ya Rhino Rangers itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mbeya City itacheza mechi yake ya kwanza kabisa ya ligi kuu katika historia yake dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine na Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Timu zilikuwa:
YANGA: Aly Mustafa (Deogratias Munishi dk.26), Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondani (Mbuyu Twite dk.15), Athumani Iddi, Simon Msuva, Salum Telela, Jeryson Tegete (Hussein Javu dk.67), Didier Kavumbagu, Haruna Niyonzima.
AZAM: Aishi Manula, Erasto Nyoni (Joakins Atudo dk.58), Nazir Salum, David Mwantika, Aggrey Moris, Himid Mao, Kipre Tchetche, Salum Abubakar, John Bocco (Gaudence Mwaikimba dk.74), Michael Balou (Ibrahim Mwaipopo dk.62), Khamis Mcha.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments: