Sumaye: Vigogo wanahusika
Asema wanawatumia vijana kufanikisha biashara hiyo
Maofisa wawili uwanja wa JNIA wasimamishwa kazi
Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amewashukia
‘vigogo’ wenye madaraka, kuwa wanahusika kushamirisha biashara ya dawa
za kulevya, wakiwatumia vijana katika kufikia malengo yao.


Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye
Sumaye amesema, mbali na ‘vigogo’ hao,
biashara hiyo inawahusisha baadhi ya wafanyabiashara wenye nguvu kubwa
za kiuchumi, na kusisitiza hakuna sababu kwa jamii kuogopa ama
kulifumbia macho tatizo hilo.
Hata hivyo, Sumaye ambaye ni kiongozi
pekee aliyehudumu wadhifa wa Uwaziri Mkuu kwa muda mrefu (miaka 10),
hakuwataja kwa majina vigogo ama wafanyabiashara hao.
Lakini katika siku za hivi karibuni,
kumekuwapo taarifa zinazowahusisha baadhi ya wanasiasa, akiwamo Mbunge
wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) ambaye hata hivyo, alikana kuhusika katika
biashara hiyo.
Pia, aliyewahi kuwa Mbunge kupitia Umoja
wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), marehemu Amina Chifupa,
aliwahi kutamka kuhusu kuwapo viongozi, wanasiasa na wafanyabiashara
wanaojishughulisha na biashara hiyo, akitaka serikali iwashughulikie.
“Hili ni tatizo ambalo hatuwezi kulifumbia
macho. Biashara ya dawa za kulevya inafanywa na watu wazito ama kwa
fedha zao au kwa madaraka yao,” alisema Sumaye.
Sumaye alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa Kituo cha Maendeleo ya vijana (Tayodec) mjini Arusha jana.
Alisema hivi sasa nchi inaonekana kuwa kituo muhimu cha kupitishia dawa hizo kwenda ama kutoka katika mataifa mengine.
“Hii siyo sifa nzuri kwa nchi yetu. Lakini
ukiachilia mbali madhara ya kupitishia nchini, dawa hizo zinawathiri
sana vijana wetu na kuwageuza mazezeta kwa baadhi ya wale wanaozitumia,”
alisema.
Kwa mujibu wa Sumaye, uhalifu mwingi wa
kutisha unafanywa na watu wanaozitumia dawa hizo, huku vijana wanatumika
kuzibeba kwenye miili yao, hali inayohatarisha maisha yao ikiwamo kufa.
“Cha kusikitisha wenye biashara hiyo wao
hawaendi kuleta hizo dawa wala hawawatumii watoto wao, bali watoto wa
wenzao ili wakikamatwa na vyombo vya dola au kudhurika kwa ubebaji huo,
iwe ni shauri yao,” alisema.
“Hii ni roho mbaya tena ya kinyama sana,
kuona wewe kupata fedha hizo chafu kwa gharama ya mtoto wa mtu mwingine,
ati ni sawa tu. Lazima tujali watoto wa wenzetu kama watoto wetu,”
aliongeza.
ASEMA ANAHUJUMIWA KWA VIJANA
Sumaye alisema Tayodec ni taasisi
inayoshughulika na vijana, ikimteua kuwa mlezi wake, lakini akipata
upinzani kutoka kwa watu wasiomtakia mema.
Alisema watu hao (hakuwataja majina), wameiona taasisi hiyo kama mtaji wa kisiasa na kutaka kuitumia kwa malengo hayo.
“Najua mmeshawishiwa kwa ahadi ya fedha
nyingi na wakati huo huo kunikejeli mimi kuwa sina fedha. Nadhani
hawakujua kuwa moja ya malengo makuu ya taasisi ni kupiga vita rushwa na
tabia ya kununua watu na mngekubali kununuliwa basi ndiyo ungekuwa
mwisho wa taasisi yenu,” alisema.

WAWILI WASIMAMISHWA JNIA
Wakati Sumaye akitoa angalizo hilo,
maofisa wawili wa kitengo cha ukaguzi katika Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, wamesimamishwa kazi kupisha
uchunguzi unaohusishwa na kukamatwa kwa dawa za kulevya nchini Afrika
Kusini.
Hivi karibuni, wasichana wawili wa
Tanzania, Agnes Jerald (25) maarufu kama Masogange na Melisa Edward
(24), walikamatwa nchini humo wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal
Methamphetamine, zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8, zikitokea hapa
nchini.
Washitakiwa hao ambao walikatwa katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo uliopo jijini Johannesburg,
wakiwa na kilo 150 za dawa hizo zilizohifadhiwa kwenye masanduku sita.
Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Poul Rwegasha,
aliimbia NIPASHE Jumapili kuwa kufuatia sakata la dawa hizo,
wamewasimamisha kazi maofisa hao ambao hakuwataja majina wala taasisi
wanazofanyia kazi, ili kupisha uchunguzi.
“Siku ya tukio hilo, tuliangalia kamera za
usalama (CCTV) na kuwaona maofisa hao, hivyo tumewasimamisha kwa ajili
ya uchunguzi na siyo kwamba wamefukuzwa kazi,” alisema.
Alisema kwa hatua hiyo, wameondolewa
kwenye kitengo cha ukaguzi, ingawa bado wanafika kazini wakati uchunguzi
dhidi yao ukiendelea.
Kwa mujibu wa Rwegasha, maofisa wawili wa polisi, ni miongoni mwa walioonekana kwenye CCTV hiyo, ingawa hakutaja majina yao.
Alisema hakuna uthibitisho wa moja kwa
moja kuhusu kuhusika kwa askari hao, hivyo uchunguzi ukikamilika hatua
zinazostahili zitachukuliwa.
“Siyo vizuri kukutajia majina ya hao
maofisa kwani utaharibu uchunguzi wetu, na bado hawajakutwa na hatia,
uchunguzi utakapokamilika nitakupatia taarifa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege,
Deusdedit Kato, alisema zaidi ya watu 10 wamehojiwa kuhusiana na tukio
hilo, na kwamba watajulikana pindi uchunguzi utakapokamili.
Mwandishi Wetu, Arusha na Beatrice Shayo, Dar
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments: