Wachezaji ligi kuu kupimwa mkojo

Wachezaji wa ligi kuu ya Bara watakuwa wakipimwa mkojo kwa kushitukizwa kila baada ya mechi katika msimu ujao ili kubaini wenye kujihusisha na matumizi ya madawa yaliyopigwa marufuku, imeelezwa.
Akizungumza jijini mwishoni mwa wiki, msemaji wa shirikisho la soka, TFF, Boniface Wambura alimsema wachezaji watakuwa wakichaguliwa bila utaratibu maalumu kila baada ya mechi kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli za kufanyiwa vipimo.
Ligi kuu ya Bara itaanza Agosti 24 kwa mechi saba zitakazozikutanisha Yanga na Ashanti, Mtibwa Sugar na Azam, JKT Oljoro na Coastal Union, Mgambo JKT na JKT Ruvu, Rhino Rangers na Simba, Mbeya City na Kagera Sugar, na Ruvu Shooting dhidi ya Prisons.
Wambura alisema jopo la madaktari wa TFF kwa kushirikiana na tabibu wa klabu husika watachagua wachezaji bila mpangilio maalumu katika mechi mbalimbali za ligi.
Wachezaji watakaochaguliwa, alisema Wambura, watachukuliwa sampuli ya mkojo kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.
Wote watakaobainika kutumia madawa yaliyopigwa marufuku michezoni, alisema Wambura, watafungiwa kwa mujibu wa kanuni zinazosimamia kosa hilo.
“Utumiaji madawa yaliyopigwa marufuku ni tatizo la dunia nzima, na kwa Tanzania pia tunayapiga vita kwa sababu yanaondoa ushindani wa haki kwenye michezo," alisema Wambura.
“Hapa nchini wachezaji wengi ambao wanatumia madawa yaliyopigwa marufuku hujihusisha na uvutaji wa bangi ambayo ni vigumu kuigundua mwilini mwa mchezaji ambaye alitumia miaka miwili au mitatu iliyopita, hivyo inahitaji kuchunguzwa kwa muda mrefu.
“Lakini TFF itaendelea kuipiga vita na nina hakika tutapunguza uvutaji bangi huu kama si kuutokomeza kabisa."
 
Wambura aliwataka wachezaji na viongozi wa klabu kuungana na TFF na FIFA, shirikisho la soka la kimataifa, kupiga vita matumizi ya madawa haramu ili kuinua ushindani wa haki kwenye mchezo huo.
Msemaji huyo wa TFF alisema shirikisho linakusudia kuwekeza zaidi kwenye elimu juu ya madhara ya madawa haramu kwenye michezo, hata hivyo, na kueleza jina la Tanzania bado ni safi katika anga ya kimataifa.
“Timu ya taifa imecheza zaidi ya mechi 10 (katika miaka miwili iliyopita), Azam na Simba zimeshiriki michuano ya klabu ya Afrika (mwaka huu) lakini hakuna mchezaji aliyegundulika kutumia madawa," alisema Wambura.
Wambura alisema katika michuano ya kimataifa maofisa wa FIFA na wa CAF, shirikisho la soka la Afrika, hufanya pia uchunguzi wa madawa haramu kwa kushitukiza mara kwa mara.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments: