Yanga waitana kujadili udhamini Azam TV

Uongozi wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga umeitisha mkutano wao mkuu wa dharura utakaofanyika Agosti 18 kwenye ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam kujadili udhamini wa kampuni ya Azam Media iliyopewa haki ya kurusha ‘live’ kupitia televisheni mechi za msimu ujao wa ligi utakaoanza Agosti 24.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kuipa haki hiyo Azam Media baada ya kukubali kuingia mkataba wa udhamini wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh. bilioni 5.56.

Akizungumza jana kwenye makao makuu ya klabu ya Yanga, Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako, alisema kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa ajenda hiyo, kamati ya utendaji ya klabu yao ilikutana na kuamua kuitisha mkutano mkuu wa wanachama.

Aliongeza kuwa wanachama ndiyo wenye haki ya kuamua kama klabu yao itambue au ikatae udhamini huo (wa Azam TV) kwa kuzingatia maslahi ya timu yao.

"Kwa kuzingatia misingi ya haki ya kidemokrasia tuliyojijengea, uamuzi wa mwisho utatokana na maamuzi ya wanachama wetu. Wao ndiyo watasema njia gani tuifuate," alisema Mwalusako.

Aliongeza kwamba bado uongozi wa Yanga unaamini kuwa udhamini huo kwao si mzuri na huenda timu yao ikahujumiwa katika mchakato wa kurusha mechi zake moja kwa moja.

Alieleza kwamba baada ya kamati ya utendaji ya klabu hiyo kufanya uchambuzi wake na kujiridhisha, iliona kuwa makubaliano yaliyofanywa kati ya kamati ya ligi na wadhamini hao hayana maslahi yoyote kwa klabu yao.

"Tunaona kuna nguvu ya ziada inatumika kupotosha msimamo wa kamati ya utendaji na kuidhalilisha klabu ya Yanga hadharani," aliongeza Mwalusako, bila kufafanua zaidi juu ya namna wanavyodhalilishwa kupitia suala hilo.

Yanga ilieleza kwamba kiasi cha fedha kilichotangazwa kupewa kwa kila klabu ambacho ni Sh. milioni 100 kwa msimu ni kidogo na hakilingani na thamani ya klabu yao.

Uongozi wa Yanga pia ulisema kwamba si sahihi fedha zitokanazo na udhamini huo kugawanywa sawa kwa klabu zote zinazoshiriki ligi wakati wao ni wakongwe na wana wanachama wengi ukilinganisha na timu nyingine zinazomilikiwa na kampuni au taasisi.

Yanga ilieleza kwamba inahitaji kuhakikishiwa kutohujumiwa kwa baadhi ya matukio ya kimchezo yatakayofanywa na wachezaji wake kwani vinginevyo yatakuwa yakionyeshwa mara nyingi na Azam Media ambao pia wana timu inayocheza ligi kuu ya Azam.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: