Kesi dhidi ya Pinda Oktoba 18

Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imesema itasikiliza kesi ya  Kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wakiomba mahakama hiyo itoe tafsiri za kisheria katika baadhi ya Ibara Oktoba 18.


Uamuzi huo ulifikiwa jana na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Kiongozi Fakihi Jundu, Dk. Fauz Twaib na Agustine Mwarija baada ya kutoa muda wa siku 14 kwa pande zote mbili kujibishana majibu ya kisheria kwa njia ya maandishi kuhusu kesi hiyo.

Kesi hiyo namba 24 ya mwaka huu  iliyofunguliwa mahakamani hapo,  hati ya mashtaka inaonyesha kwamba washtakiwa katika kesi hiyo ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mawakili wanaomtetea Pinda na Mwanasheria Mkuu ni, Mawakili wa Serikali Wakuu,  Nickson Mtimbwa, Sara Mlipano na Alesia Mbuya.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na Mawakili Fulgence Massawe, Haroud Sungusia wa LHRC,  Francis Stolla, Mpare Mpoki,  Peter Kibatala na Jeremia Mtobezwa, kutoka Chama Cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS).

Katika hati ya kupinga maombi hayo, walalamikiwa (Pinda na Mwanasheria Mkuu),wamedai kuwa kesi hiyo haipo kisheria na kwamba inakwenda kinyume cha katiba na ile sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge.

Sababu ya Pili, kesi hiyo haina msingi inapingana na sheria namba 6 kanuni namba 3 ya mwenendo wa makosa ya madai na amri ya 28  kanuni ya kwanza ya sheria hiyo.

Walalamikiwa kupitia hati hiyo wamedai kuwa sababu ya tatu, kesi hiyo hieleweki inasababisha usumbufu kwa kuwa inapingana na sababu ya madai na haki za msingi.

Pinda analalamikiwa kuwa wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge alitoa maelekezo kwa Jeshi la polisi kuwapiga watu wote wanaokaidi maagizo ya jeshi la Polisi.

CHANZO: NIPASHE

0 comments: