Wafanyabiashara wengine mbaroni kesi ya mauaji ya bilionea Msuya

Sakata la mauaji ya mfanyabiasha bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43), limechukua sura mpya baada Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kuwashikilia wafanyabiashara wengine wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara huyo.


Waliokamatwa katika sakata hilo ni Joseph Damas maarufu kama ‘Chusa’ (35), ambaye ni milionea wa madini ya Tanzanite na mmiliki wa mgodi wa madini hayo, mkazi wa Arusha, Jalila Zuberi Saidi (28), mkazi wa Babati, Manyara, Sadiki Jabiri (32), mkazi wa Lang’ata, Wilaya ya Hai, mkazi wa Dar es Salaam na Karimu Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, wilayani Siha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Watuhumiwa hao wanne walikamatwa katika Kijiji cha Sikonge, mkoani Tabora, Septemba 13, mwaka huu, wakiwa kwa mganga wa kienyeji wakitafuta dawa na kufanyiwa zindiko, ambalo litawafanya wasinaswe na polisi wala kutajwa na wenzao.

Kamanda Boaz alisema watuhumiwa hao walibainisha kupatikana kwa silaha iliyotumika katika mauaji hayo, pamoja na pikipiki iliyotumika aina ya Kinglion yenye namba za usajili  T 751 CKB, ambayo wakati wa tukio iliwekwa namba za bandia.

“Silaha hiyo aina ya SMG yenye namba za usajili KJ 10520 ilipatikana katika Kijiji cha Boloti, kilichopo mpakani na Wilaya ya Siha na Hai, mkoani Kilimanjaro, katika eneo la Tindiga lenye majani marefu na pikipiki  ikiwa imehifadhiwa nyumbani kwa mtu,” alisema Kamanda Boaz.

Watuhumiwa hao waliokamatwa mkoani Tabora, wanafikisha idadi ya watuhumiwa saba waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji ya bilionea Msuya, wataunganishwa katika kesi ya mauaji namba 6 ya mwaka 2013 iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro, Munga Sabuni.


Alisema upelelezi unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa hao wanne watafikishwa mahakamani na kuungana na wenzao katika kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa.

Hata hivyo, kesi hiyo imepangwa kutajwa kesho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi iliyopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Msuya aliuawa Agosti 6, kwa kupigwa risasi kwa kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), eneo la Mjohoroni kati ya mji wa Bomang’ombe na makutano ya Barabara ya KIA.

Washtakitwa wengine ni Sharifu Mohamed Athumani (31), ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandulu, mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Said maarufu kama ‘Mredi’ (38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Somanjiro na Musa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai Kwa Mrefu, mkoani Arusha.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: