Kiwanda cha silaha chagundulika Morogoro
Kiwanda
bubu cha kutengeneza silaha za aina mbalimbali ikiwemo bunduki aina ya
gobore na bastola, kimebainika kuwepo kati kati ya mji wa Morogoro,
katika eneo la kwa Mavumila.
Eneo hilo ni maarufu kwa utengenezaji wa funguo, ambapo watu kadhaa wamekamatwa na wanahojiwa na polisi kutokana na tukio hilo.
Waandishi wa habari waliofika eneo la
tukio, walishuhudia ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa eneo la Masika,
mtaa wa Kingo, kwenye nyumba ya marehemu Mavumila, ambayo imekuwa
maarufu kutokana na matengenezo ya funguo.
Polisi kwa kushirikiana na kikosi cha
kuzuia ujangili, idara ya wanyamapori, wamegundua kiwanda bubu cha
kutengeneza silaha, na kukuta mitambo, malighafi na silaha
zilizokamilika ikiwemo bunduki kadhaa zilizokamilika na ambazo zilikuwa
bado katika matengenezo, kwenye nyumba hiyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kingo, Mwajuma
Ndege, aliyekutwa eneo la tukio, alieleza kushangazwa na hali hiyo,
ingawa alikiri miaka ya nyuma eneo hilo lilitumika kwa matengenezo ya
funguo, sambamba na kusafisha magobore.
Ndege alisema suala la kuwepo kwa kiwanda
hicho bubu huku majirani wakiwa hawafahamu, ni hatari kwa hali ya
kiusalama, na kwamba hata yeye kama kiongozi wa mtaa, hakudhani kama
kuna kiwanda kilichosheheni mitambo na malighafi za hatari namna hiyo.
Naye Ernest Mhando, mkazi wa Morogoro,
alisema kiwanda hicho ni cha muda mrefu, na kimekuwa kikitumiwa kwa
matengenezo ya funguo hivyo, lakini ili kuhakikisha usalama wa
watanzania ni vyema wanaohusika na usajili wa viwanda wakaweka wazi
iwapo kina uhalali wa kutengeneza silaha.
Watuhumiwa kadhaa wameweza kutiwa mbaroni
katika tukio hilo, ingawa kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Faustine
Shilogile, aliahidi kukutana na waandishi wa habari siku ya Jumapili,
kwaajili ya kutolea ufafanuzi kuhusiana na kiwanda hicho bubu cha
silaha.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments: