Mchakato sheria dhidi ya dawa za kulevya waanza

Mchakato wa kuanzisha sheria mpya ya kudhibiti dawa za kulevya umeanza kuiva, baada ya serikali kupeleka sheria ya zamani katika vyuo vikuu vya sheria na katika taasisi zisizokuwa za kiserikali ili wadau waichambue na kutoa maoni yatakayowezesha kupatikana kwa  sheria madhubuti itakayokidhi hali halisi ya kukabiliana na tatizo hilo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, akizungumza jana katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, alisema serikali imejipanga kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka huu sheria hiyo mpya iwe imekamilika.

Alisema hatua ya serikali kuamua kutunga sheria mpya ni baada ya kuona sheria iliyopo haikidhi kikamilifu udhibiti wa tatizo la dawa za kulevya nchini pamoja na kusababisha uamuzi katika baadhi ya kesi hizo kuacha hisia mbaya na malalamiko mengi toka kwa  jamii dhidi ya serikali.

"Serikali imeamua kushirikisha wadau wengi kwa kuwa wana uelewa wa kutosha kuhusu tatizo la dawa hizo ili waweze kuchambua sheria iliyopo na kutoa michango, maoni na ushauri utakaowezesha kupatikana kwa sheria madhubuti itakayokidhi hali halisi ya tatizo na kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulenya nchini," alisema.

Alitaja upungufu uliopo katika sheria iliyopo kwa kutoa mifano ya kifungu cha 21 kinachohusu wafadhili wa biashara hiyo kupewa adhabu ndogo licha ya kuwa ndio wamiliki na wanaostahili adhabu kali.

Alisema adhabu iliyopo ni faini ya Sh. milioni 10 au kifungo cha maisha jela, huku ikimpa uhuru jaji au hakimu kutoa uamuzi wa kifungo au kumtoza faini mtuhumiwa kadri anavyoona inafaa jambo ambalo kutokana na kukithiri kwa biashara hiyo inakuwa rahisi kulipa.

Alisema mkoa wa Arusha ndio unaoongoza kwa biashara hiyo haramu ambako walikamatwa watuhumiwa 144, Dar es Salaam 90, Tanga 37, Kilimanjaro 17, Mbeya 13, Morogoro 9 na Mara wanne.

CHANZO: NIPASHE

0 comments: