Ponda anyimwa dhamana

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imemnyima dhamana Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, anayekabiliwa na mashtaka ya kukaidi amri halali, kuharibu imani za dini na kushawishi na kutenda kosa.


Mahakama hiyo iliamua kumnyima dhamana Shekh Ponda jana baada ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Richard Kabate, kupitia vifungu mbalimbali vya sheria na kukubaliana na ombi la Mkurugenzi Mshtaka (DPP) lililowasilishwa mahakamani hapo Agosti 28, mwaka huu kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya pili.

Ombi hilo lilitolewa na Wakili wa Serikali,  Bernad Kongola, akidai kuwa DDP amezuia mshtakiwa huyo kupewa dhamana  kwa sababu ya maslahi ya nchi na usalama wake mwenyewe.

Baada ya Shekh Ponda kunyimwa dhamana wakili wake, Juma Nassoro, aliwasilisha ombi jingine mahakamani hapo la kufuta shitaka la kwanza ambalo ni kukaidi amri halali akidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza  vinginevyo lifunguliwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Akitoa sababu za kutaka kufutwa ama kuhamishia shtaka hilo katika Mahakama ya Kisutu, Wakili Nassoro, alidai kuwa amri hiyo halali anayodaiwa kuivunja mteja wake ilitokana na hukumu iliyotolewa katika Mahakama ya Kisutu Mei mwaka huu ambayo Ponda alihukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja na kutotakiwa kufanya kosa lolote la jinai katika kipindi cha mwaka mmoja.

Ombi hilo lilisababisha mvutano wa kisheria kati ya upande wa mashitaka na upande wa utetezi hali iliyomfanya Hakimu Kabate kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba mosi, mwaka huu ili kupitia vifungu mbalimbali vya kisheria ambavyo vitatoa maamuzi endapo mahakama yake itakuwa na uwezo wa kusikiliza shitaka hilo ama shitaka hilo lifunguliwe katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Pia upande wa mashitaka kupitia Wakili wa Serikali, Sunday Hiela, waliwasilisha hati yenye maelezo ya mlalamikaji wa kesi hiyo ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo iliombwa na wakili wa upande wa utetezi.

ULINZI WAIMARISHWA
Ponda alifikishwa mahakamani hapo mapema jana asubuhi saa 2:30 tofauti na siku nyingine kwa kutumia usafiri wa basi la Jeshi la Magereza lililoongozwa na magari matano huku ulinzi mkali ukiimarishwa katika eneo la mahakama hiyo.

Katika eneo la Mahakama walitanda askari polisi wakiwamo makachero na wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kikosi maalum cha askari Magereza waliokuwa na silaha za moto, mabomu ya machozi, mbwa, virungu na zana nyingine.

Mbali ya kuimarishwa ulinzi katika eneo la Mahakama, pia barabara zinazokatisha mahakamani hapo zilifungwa hali iliyosababisha kusimama kwa muda kwa shughuli katika ofisi za serikali zilizopo mahakamani hapo ikiwamo ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ofisi ya Hazima Ndogo na Madini.

Hatua ya kufunga kwa ofisi hizo ilitokana na watu wanaodhaniwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda kuwasili katika eneo hilo la mahakama kuanzia majira ya saa 1:00 asubuhi wakidaiwa kutoka katika mkesha  kwenye msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja uliopo  eneo la Kiwanja cha Ndege kwa ajili kusoma  itikafu kubwa ya kitaifa.

Itikafu hiyo iliyosomwa juzi usiku ilishirikisha  Masheikh kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Tanga, Arusha na Dar es Salaam.

Idadi kubwa ya wafuasi wa Shekh Ponda walionekana nje ya uzio wa mahakama hiyo huku baadhi ya wanawake wakionekana kulia na wengine kusema takbir (Tukuza), Allaahu Akbar (Mungu ni mkubwa) na baada ya kuhairishwa kwa kesi hiyo wafuasi hao walimsindikiza Ponda mita chache kutoka katika viunga vya mahakama hiyo.

juzi kuanzia saa 9:00 usiku hadi jana asubuhi, Waislamu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Sheikh Ponda walihudhuria itikafu iliyosomwa kwa ajili ya kumuomba kiongozi huyo ashinde kesi inayomkabiri.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: