Serikali kuziongezea mikopo sekta binafsi

Serikali imesema itaendelea kuziwezesha sekta binafsi nchini ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 na kuchagiza ukuaji wa haraka wa uchumi wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kuhusu ushiriki wa sekta binafsi
katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo 2013/2014, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini kutoka Tume ya Mipango, Joyce Mkinga, alisema kuwa, katika kufikia lengo hilo serikali imedhamiria kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kufikia asilimia 20 ya pato la taifa kufikia Juni mwakani, lengo likiwa ni kuziwezesha kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa mwaka 2013/2014, serikali inatilia mkazo ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji kwenye miradi mbalimbali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na kuziwezesha kukopa na kuchangia maendeleo ya nchi,” alisema.
Alisema kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kuisaidia serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye mpango wa utekelezaji wa miaka mitano kutoka 2011 hadi 2016.

Vipaumbele katika mpango huo ni miundombinu, kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu, uendelezaji wa huduma za utalii, biashara na fedha.

Kwa mujibu wa Mkinga, hatua mbalimbali zimechukuliwa na serikali katika kuhakikisha kunakuwapo na ufanisi kwenye masuala ya ubia baina ya sekta za umma na  binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kukamilisha mwongozo wa utekelezaji wa sera, sheria na kanuni kati ya sekta hizo.
Alitaja baadhi ya  mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 kuwa ni pamoja na kusajiliwa kwa miradi ya viwanda 186, kati ya hiyo, 157 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), huku 29 ikiwa imesajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji (EPZA).

Naye Mchumi Mwandamizi katika Tume ya Mipango, Andrea Aloyce, alisema, sekta binafsi ni za muhimu kwani serikali pekee haiwezi kutekeleza mipango na miradi yote ya maendeleo bila hizo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: