Lema fupa gumu
Polisi walifanya uvamizi huo usiku wa manane Aprili 25, mwaka huu baada ya awali kumta Mbunge huyo ambaye amekuwa kwenye mapambano makali ya kisiasa jimboni kwake, ajisalimishe kwa madai ya kuwahamasisha wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kumzomea Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Kutokana na kadhia aliyokutana nayo Mulongo IAA alitoa amri ya kukamatwa kwa Lema, amari ambayo polisi waliibeba nzima nzima kiasi cha kuruka ukuta wa nyumba yake na kuvunja milango usiku na kumfunga pingu kama muhalifu sugu.
Lema alifutiwa kesi hiyo jana baada ya upande wa mashtaka kusema hauna nia ya kuendelea na kesi iliyokuwa inamkabili ya kufanya uchochezi kwa wanafunzi wa IAA, ambao licha ya kumzomea Mulongo walisababisha kuzuka kwa vurugu.
Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Devotha Msofe wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, lakini baada ya kuingia mahakamani hapo, Wakili wa Serikali, Elianenyi Njiro, aliiomba mahakama ifutwe kesi hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kama ilivyorekebishwa 2002.
“Mheshimiwa, upande wa mashtaka umeona kuwa hauna nia ya kuendelea na hili shauri, tunaiomba mahakama yako kuifuta chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,” alisema.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Hakimu Devotha alikubaliana nalo na akamweleza mshtakiwa kuwa yupo huru kuanzia muda huo.
“Mshtakiwa upo huru kuanzia sasa, lakini kama upande wa mashtaka utaona kuna haja ya kuendelea na shauri hili unaweza kukamatwa, lakini kwa sasa mahakama inakuachia huru,” alisema na kumaliza shauri hilo.
Wakili Method Kimomogoro, anayemtetea Lema aliwakilishwa mahakamani hapo na wakili John Lundo.
Akisomewa maelezo ya awali Julai 10 mwaka huu mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Elianenyi alidai Aprili 24 mwaka huu, Lema akiwa eneo la Freedom Square la IAA alifanya kosa la uchochezi wa kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Akifafanua shtaka hilo, Elianenyi alidai kuwa Lema aliwaeleza wanafunzi wa chuo hicho ambao walikuwa wamekusanyika kufuatia kuuawa kwa mwenzao na watu wasiojulikana kuwa:
“Mkuu wa Mkoa amekuja kama anakwenda kwenye send-off, hajui Chuo cha Uhasibu mahali kilipo wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hiki. Ameshindwa kuwapa pole kwa kufiwa na kusikiliza shida zenu na amesema hawezi kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu.”
Upande wa mashtaka unadai kuwa kauli hiyo iliwafanya wanafunzi kurusha mawe na chupa wakati Mkuu wa Mkoa Mulongo alipokuwa akitoa hotuba yake kwa wanafunzi hao hali ambayo ilisababisha uvunjifu wa amani chuoni hapo.
Upande wa mashtaka tayari ulikuwa umewaleta mashahidi watano ambao ni Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Giles Mroto, Naibu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Faraji Kasidi, Inspekta wa Polisi Bernard Nyambalya, Jane Chibuga na Mwadili Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, John Joseph Nanyaro.
NJE YA MAHAKAMA
Akizungumza nje ya mahakama baada ya kesi yake kufutwa, Lema alisema: “nilikuwa najua kesi hii ilikuwa ya kutengenezwa na ndiyo maana mashahidi wengi walikuwa polisi.”
Alidai kuwa hata Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Arusha ambaye awali alitakiwa kutoa ushahiri upande wake, baadaye alimruka na kuhamia upande wa mashtaka ambako alitakiwa kutoa ushahidi dhidi yake.
Alidai kuwa kosa aliloshtakiwa ni la ‘kitoto’ sana kwa madai ya kumwambia Mkuu wa Mkoa kuwa alikwenda kuonana na wanafunzi waliofiwa na mwenzao kama vile anakwenda kwenye send-off.
Hata hivyo, alisema iwapo upande wa mashtaka ungeendelea na kesi hiyo, alijiandaa kupambana nayo hata kama ingechukua miaka mitano.
Alisema siku ile ambayo mwanafunzi wa chuo hicho alikufa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana, Mkuu wa Mkoa alitakiwa aonekane akionyesha umakini wa utawala.
“Wanaweza kulifuta shauri hili kama walivyofanya, lakini kesho wakatufungulia kesi nyingine, tupo tayari na mapambano yanaendelea.
“Wanataka kutuelekeza cha kufanya au tuwe waoga, sasa hivi wameyafungia magazeti mawili ili kuyatisha, sisi tunasema hatuwezi kutishika,” alisema.
KAULI YA CHADEMA
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema kufutwa kwa kesi dhidi ya Lema kunaelezea jinsi watunga hila wanavyoanza kuaibika taratibu.
“Nipo Uingereza kuhudhuria mkutano wa chama cha Conservative, nimepata taarifa ya ushindi wa kesi ya Lema, hali hii inaonyesha taratibu watunga hila wanaanza kuaibika.
“Kesi nyingi ambazo zimekuwa zinatungwa dhidi yetu kwa kweli zimetuongezea akili zaidi na mapenzi mema kwa Watanzania maana tumejigundua kuwa hata tufanywe nini bado nia na shauku yetu ya kuwatumikia Watanzania iko pale pale.
ILIVYOKUWA
Aprili 25, 2013, Jeshi la Polisi linamsaka Lema kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu zilizotokea juzi katika Chuo cha Uhasibu Mkoani Arusha na kusababisha chuo hicho kufungwa kwa muda usiojulikana.
Kaimu Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Arusha, Ibrahim Kilongo, aliwaaambia waandishi habari kuwa jeshi hilo limetoa ilani kwa mbunge huyo kujisalimisha polisi haraka.
“Tunamtaka popote alipo afike mwenyewe polisi na bado tunaendelea kumtafuta popote alipo, ni muhimu afike tufanye naye mahojiano kuhusu yaliyotokea katika Chuo cha Uhasibu,” alisema Kilongo.
Baada ya kutulizwa kwa vurugu hizo, Mulongo aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata Lema kwa kile kilichoeleza kuwa ni kumhusisha na vurugu zilizotokea chuoni hapo.
Hata hivyo, Mbunge huyo alikana vikali kuhusika katika vurugu zozote na kueleza kuwa alitumia nafasi yake kuwashawishi wanafunzi kurudi chuoni na kisha akawasiliana na Mkuu wa Mkoa kufika kuzungumza na wanafunzi hao.
Katika tukio hilo lililosababisha mabomu ya machozi kurindima kwa muda katika viunga vya chuo hicho Mkuu huyo wa Mkoa alijikuta akizomewa baada ya kushindwa kuhutubia mamia ya wanafunzi baada ya kukosekana kwa kipaza sauti.
Awali wanafunzi hao walitaka kuandamana kuelekea kituo kikuu cha polisi kufuatia mwanafunzi mwenzao kuuawa katika mazingira waliyodai yana utata karibu na chuo hicho.
Tukio hilo lilizua uhasama kati ya Mulongo na Lema huku Lema akidai kuwa alikuwa akitumiwa ujumbe wa vitisho kutoka kwa Mulongo akimtishia kwamba atamshughulikia. Hata hivyo, Mulongo alikuwa akikanusha madai hayo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments: