Serikali yayajia juu MWANANCHI, Rai

Serikali imesema imebaini kuwa baada ya gazeti la Mwananchi kufungiwa, limeendelea kuchapishwa kwenye mtandao wa internet, hivyo imeutaka uongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuacha kufanya hivyo mara moja, vinginevyo italifungia katika muda usiojulikana au italifuta kabisa.

Mbali na kuutaka uongozi wa MCL kufanya hivyo, pia imeutaka uongozi wa Kampuni ya New
Habari (2006) kuacha mara moja kuchapisha gazeti la Rai kila siku kwa kuwa limesajiliwa kutoka mara moja kwa wiki.

Agizo hilo lilitolewa na serikali kupitia Msemaji wake, Assah Mwambene, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema tayari wamekwisha kuuandikia barua uongozi wa MCL kuutaka ueleze sababu za kuchapisha gazeti, ambalo limefungiwa na serikali.

Mwambene alisema pia wameuandikia barua uongozi wa New Habari (2006) kuutaka ueleza sababu hizo.

Alisema iwapo uongozi wa MCL utashindwa kutoa maelezo yanayoridhisha, serikali italazimika kulichukulia gazeti hilo hatua kali zaidi, ikiwamo kuliongezea adhabu zaidi, ikiwamo ama kulifungia kwa muda usiojulikana au kulifuta kabisa.

Mwambene alisema kwa upande wa Kampuni ya New Habari (2006), baada ya kulifungia gazeti lake la Mtanzania, imeanza kuchapisha Rai kila siku tangu Septemba 29,  mwaka huu, bila kibali cha Msajili wa Magazeti.

Alisema gazeti la Rai ni la wiki, ambalo hutoka kila Alhamisi, hivyo kulichapisha kila siku ni kosa.
Kutokana na hali hiyo, aliutaka uongozi wa kampuni hiyo kuacha mara moja kuchapisha gazeti hilo kila siku, badala yake warudie kufuata ratiba yao hadi hapo maamuzi mengine yatakapofanyika.

Aliutaka umma kufahamu kuwa serikali haikukurupuka kuyafungia magazeti hayo, akisema uamuzi ulifanyika baada ya kufuata taratibu zote za msingi, ikiwamo kuwasikiliza wahusika.

Alisema barua zilizoandikwa kwa kampuni hizo, wanatarajiwa kujibiwa kesho, hivyo akawataka waandishi kutotumia uhuru wa habari vibaya.

Magazeti hayo yalifungiwa Septemba 27, mwaka huu, baada ya kutuhumiwa kuchapisha habari za uchochezi na uhasama.

Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kwa muda wa wiki mbili, wakati lile la Mtanzania limefungiwa kwa muda wa miezi mitatu au siku 90, kuanzia tarehe hiyo.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa New Habari 2006 Ltd, Hussein Bashe, akizingumza na NIPASHE alisema kuwa anashanzwa na maamuzi ya serikali kwa kuwa wana kibali cha kuchapisha Rai kila siku ambacho kilitolewa na Msajili wa Magazeti tangu Desemba 22, 1994.

Alisema wanashangaa serikali kudai kuwa kibali hicho kilikuwa kwa ajili ya Kampuni ya Habari Corporation na siyo New Habari 2006 Limited, ilihali inajua kuwa mali na madeni yote ya Habari Corporation vilinunuliwa na kampuni ya sasa.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Waandishi wa Habari Kimataifa (IFJ) limeeleza kusikitishwa kwake na kuendelea kukandamizwa kwa uhuru wa habari nchini hasa kufuatia kufungiwa kwa magazeti hayo wiki iliyopita.
CHANZO: NIPASHE

0 comments: