Serikali yavunja Idara Muwsa kwa ufisadi

Serikali imeivunja Idara ya Manunuzi na Usambazaji ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka   Moshi (Muwsa) kwa tuhuma za kukithiri kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Mhandisi, Syprian Luhemeja aliiambia NIPASHE jana kuwa hatua hiyo ina lengo la kuongeza mapato na kupunguza athari za kiuchumi kwa wakazi wa Moshi na miji ya jirani ya Wilaya ya Hai na Moshi Vijijini.

Uamuzi huo umetolewa ikiwa ni wiki moja tu,  tangu Naibu Waziri wa Maji, Dk.Binilith Mahenge kuhitimisha ziara yake katika wilaya sita za Mkoa wa Kilimanjaro ya  kuhamasisha uharakishwaji wa utekelezaji wa miradi ya maji kwenye vijiji 10 vilivyoteuliwa hadi kufikia mwishoni mwa Septemba mwaka huu.

Mbali ya kuivunja idara hiyo na kuiunda upya, pia imefuta mgawo wa maji kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi na wilaya jirani za Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kufanya mabadiliko makubwa katika udhibiti wa rasilimali, miundombinu na fedha za umma.

“Nimeivunja idara ya manunuzi na usambazaji na kisha kuisuka upya kwa kuzitenganisha ili ziweze kumudu kasi tuliyonayo kupitia Wizara ya Maji.

Big result now si lelemama inahitaji mikakati ambayo itaimarisha utoaji huduma,”alisema Luhemeja.

Wakazi wa Moshi walikuwa wakihaha kwa miaka kadhaa kusaka maji usiku na mchana na kuathiri ndoto za mji huo kuwa Jiji ifikapo mwaka 2015 kutokana na kuzorota kwa shughuli za kiuchumi zinazotegemea maji.


“Tumedhibiti mgawo wa maji kwa asilimia 28 kwa hiyo  Mamlaka inatangaza hakuna tena mgawo kuanzia sasa, maji yanapatikana kwa saa 24. Hii ndiyo Big Result Now (Mabadiliko makubwa na ya haraka) kuelekea kuwa Jiji la Moshi,”alitamba.

Katika kudhibiti rasilimali, fedha za umma na uboreshaji wa huduma, Mamlaka hiyo imewataka wakazi wa Moshi na maeneo ya miji ya jirani na mji huo kuanza kulipa ankara za maji kwa njia ya mitandao ya simu za mikononi ya M-pesa,Tigo Pesa, Airtel Money na Easy-Pesa ili kuepuka msongamano katika kupata huduma.

“Kikubwa tunachosisitiza hapa ni kwamba wananchi hawatakiwi kulipa madeni yao ya nyuma kwa kutumia mitandao hiyo,”alisema Luhemeja.

Kuhusu malalamiko kwenye maeneo yenye miinuko kutopata huduma ya maji hususani miji ya Rau na Kiboriloni, Mkurugenzi huyo, alisema  Muwsa imetoa Sh. mililioni 46 kuboresha miundo mbinu inayotoa huduma katika maeneo hayo.

CHANZO: NIPASHE

0 comments: