Kufuatia
matukio mfululizo ya kukamatwa kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya
wanaodaiwa kuwa ni Watanzania kwenye viwanja vya ndege nje ya nchi
wakipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema atalishughulikia suala hilo
kama alivyofanya bandarini.
Dk. Mwakyembe ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana na Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege nchini (TAA), alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es
Salaam wakati wa mazungumzo maalumu na NIPASHE kuhusu ufuatiliaji wa
vitendo hivyo vinavyoharibu taswira ya nchi kimataifa.
Alisema anafahamu kila kitu kuhusu matukio ya dawa za kulevya, lakini
anasubiri mamlaka zilizo chini yake kama vile TAA na bodi yake, uongozi
wa JNIA na Polisi, ili wafurukute kwanza kama alivyofanya bandarini kwa
lengo la kupima utendaji wao wa kazi.
“Mamlaka ni ‘system’, ina ngazi zake, kuna Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
na bodi yake, kuna polisi, kuna uongozi wa uwanja wa ndege. Nataka
muwabane kwanza hao ili wawaeleze hayo (ma)dawa ya kulevya yanapitaje
hapo? Mimi najua kila kitu kuhusu kinachoendelea na iwapo wanawazungusha
njooni kwangu,” alisema Mwakyembe na kuongeza:
“Haiwezekani ukaenda moja kwa moja kwa Rais, iwapo kuna suala
linalomhusu Waziri, atakushangaa na kukuona huelewi kitu. Najua hatua
ilipofikia na iwapo kuna mamlaka haijachukua hatua yoyote, mimi
nitaishughulikia. Na kama imepita kote na imefikia kwa DPP, najua
imefika ngazi ya kiwizara, ni lazima tulishughulikie.”
Dk. Mwakyembe aliongeza kuwa, anajua mtandao wa dawa za kulevya ni
mrefu, lakini atashughulikia kama alivyofanya katika Mamlaka ya Bandari
nchini (TPA), kwani baada ya kusikia ubovu unaotendeka aliwaacha
wafurukute kwanza kwa takribani wiki mbili.
Alisema baada ya wiki hizo mbili akiwa na taarifa kamili kuhusu
kilichokuwa kinaendelea, aliingia bandarini hapo na kuwafumua baadhi ya
watendaji na kwamba ndivyo itakavyokuwa katika mamlaka zinazohusika na
viwanja vya ndege kwani kwa sasa anasuburi kuona wanafanya nini kabla
hajaingilia kati.
Agosti 27, mwaka jana, Waziri Mwakyembe aliunda Kamati ndogo ya
Uchunguzi ya watu saba kubaini chanzo cha matatizo yanayozorotesha
ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kukimbiwa na wateja wa
ndani na nje ya nchi.
Baada ya uchunguzi huo, Dk. Mwakyembe aliwaondoa wajumbe wote wa Bodi ya
TPA na kuteua wapya ili kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa
taarifa hiyo.
Juzi gazeti hili liliwasili katika ofisi za TAA, kwa lengo la kujua
kinachoendelea kuhusu matukio hayo, lakini mmoja wa wafanyakazi katika
ofisi hizo alisema Mkurugenzi wa mamlaka hiyo yupo, lakini asingeweza
kuzungumza na waandishi bila kuruhusiwa kwanza na katibu wake wa mambo
ya sheria, Ofisa Uhusiano na mwingine wa tatu ambao nao hawakuwapo hapo
ofisini.
Mfanyakazi huyo wa kike ambaye alikataa kutaja jina lake wala cheo
chake, alisema ofisi ya Mkurugezni ina watu watatu na utaratibu
uliowekwa ofisini hapo ni kwamba, iwapo wafanyakazi hao wote hawapo,
hakuna huduma itakayotolewa kwa mtu mwenye shida na Mkurugenzi kwa kuwa
hataruhusiwa kumwona.
Hata hivyo, NIPASHE ilifanikiwa kumwona Mkurugenzi wa JNIA, Moses
Malaki, ambaye naye alidai kwamba, hawezi kuzungumzia sakata hilo kwa
madai kwamba hashughulikii masuala ya dawa za kulevya.
Malaki alisema wanaohusika na suala hilo ni polisi kwa kuwa JNIA
wanahusika na masuala ya wasafiri na kwamba anayeweza kuzungumzia sakata
hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Suleiman Suleiman.
Wakati wa mazungumzo na gazeti hili ofisini kwake siku hiyo, Malaki,
alimpigia simu Suleiman ambaye aliahidi kukutana na NIPASHE jana saa 5
asubuhi ili kutoa ufafanuzi wa sakata hilo.
Hata hivyo, jana mwandishi wa habari hizi alikwenda ofisini kwa
Mkurugenzi huyo na kutaarifiwa kwamba amsubiri kidogo kwa sababu yupo
kwenye kikao.
Hata hivyo, baada ya kusubiri kwa saa nne, katibu muhtasi wa mkurugenzi
huyo alimweleza mwandishi kwamba bosi wake amekataa kuzungumzia jambo
hadi atakapokuwa tayari.
"Mkurugenzi amesema hawezi kuzungumza tena na wewe hadi atakapopata muda
wa kuongea na waandishi wa habari," alisema katibu ambaye hakutaja jina
lake.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini,
Deusdedit Kato, alisema kuwa, tayari wameshaandaa jalada la matukio hayo
na juzi walilipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya
hatua zaidi za kisheria.
Hata hivyo jana, NIPASHE ilifika ofisini kwa DPP na kupewa taarifa ya
kwamba yupo Dodoma kwa shughuli za kikazi hivyo msaidizi wake hawezi
kuzungumzia lolote hadi yeye atakaporudi.
Julai 5, mwaka huu wasichana wawili wa Kitanzania walikamatwa nchini
Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine
kilo 150 zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8, zilizokuwa zikisafirishwa
kutoka Tanzania.
Wasichana hao ambao ni Agness Gerald (25) na Melisa Edward (24),
walikamatwa nchini humo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, uliopo
eneo la Kempton Park.
Ijumaa wiki iliyopita, taarifa kutoka Hong Kong, zilieleza kwamba
maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Hong Kong (HKIA),
walimkamata kijana mwenye umri wa miaka 25 akitokea Tanzania akiwa na
dawa na za kulevya aina ya heroine kilo 1.6 zenye thamani ya Sh. bil.1.5
kwenye mzigo wake wa mkononi.
Taarifa zinaeleza zaidi kwamba, maofsa hao jioni siku hiyo hiyo
walimkamata Mtanzania mwingene mwenye umri wa miaka 45 ambaye alipelekwa
hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa aina ya heroine.
Mbali na hilo, pia Mtanzania mwingine mwenye miaka 28 alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.
Matukio hayo yametokea ikiwa ni takribani wiki moja baada ya Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, Juni 28, mwaka huu kutangaza kuwa tatizo la dawa za
kulenya hivi sasa ni janga la kitaifa.
Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika
biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba,
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa
kwa kujihusisha na dawa hizo.
Pia alisema katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi
za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, na hivyo kuharibu taswira ya nchi
na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti
magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
0 comments: